Sunday, July 24, 2016

CHUNGU, TAMU MIEZI 32 YA MALINZI TFF


ZIMEBAKI siku 98,  Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, atimize miaka mitatu tangu aiingie madarakani usiku wa kuamkia Oktoba 28, 2013 kuliongoza shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka nchini.
Kuna mambo mengi yanayohusu soka la Tanzania yaliyofanyika katika kipindi hiki cha miezi 32 na siku 27 cha uongozi wa Malinzi, lakini sehemu kubwa ya mipango na uamuzi uliofanya na utawala wa rais huyo haukuwa na tija kwa maendeleo ya mchezo huo nchini tena huenda ukawa hauambatani na sera za utawala bora.
Makala haya yanaangalia baadhi ya mambo mabaya na mazuri yaliyofanywa na uongozi wa Malinzi tangu aingie madarakani kumrithi mtangulizi wake, Leodegar Tenga. Swali kubwa ambalo mdau wa soka nchini anaweza kujiuliza ni je Utawala bora kwa Malinzi uko wapi?
TFF YAMSHINDWA JERRY MURO
Mnamo Oktoba 19, 2011 kwenye mkutano wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) uliofanyika Zurich, Uswisi ukiongozwa na Mkurugenzi wa wanachama na maendeleo ya FIFA, Thierry Regenass, kamati ya utendaji na viongozi wa mashirikisho ya soka ulizokutanisha nchi wanachama. Lengo la mkutano ulikuwa ni wa FIFA kueleza marais wa mashirikisho kuwa wana mamlaka ya kusimamia soka kwa kuzingatia sheria lakini kwa nafasi ya kufanya chochote.
Rais wa TFF, Malinzi ni kama ameshindwa kutambua hilo haswa kwenye sakata linalomuhusu msemaji wa Yanga, Jerry Muro ambaye hivi karibuni ameonekana kuwa na ubavu mkubwa zaidi ya shirikisho hilo.
Julai 7 mwaka huu, Kamati ya maadili ya TFF chini ya mwenyekiti wake, Wilson Ogunde ilimfungia Muro kujihusisha na mambo ya soka kwa mwaka mmoja na faini ya milioni tatu lakini msemaji huyo aliidindia TFF siku hiyo hiyo na kusema kuwa shirikisho hilo.
Inashangaza kuwa licha ya kuwa kuna zaidi ya wasemaji wa klabu 50, yaani wa timu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL), Muro ndiyo msemaji pekee ambaye amekuwa akiishambulia TFF kwenye vyombo vya habari kwa kigezo kuwa hawawezi kumwambia kitu kwa kuwa TFF haijamuajiri.
Muro alipelekwa kwenye kamati ya maadili akituhumiwa kupingana na maamuzi pamoja na kuishambulia TFF kwenye vyombo vya habari.
Moja ya kauli ya muro kwa TFF baada ya kusimamishwa, “TFF haiwezi kuniambia niache kuzungumzia klabu yangu, TFF haijaniajiri na hainilipi mshahara. Mwajiri wangu ndiye anayeweza kuniambia nisizungumze kwasababu  hao ndiyo walioniweka pale wakijua mimi ni mtu makini.
AMUUNGA MKONO MTUHUMIWA WA ‘RUSHWA’
Desemba 2014, TFF chini ya Malinzi  iliweka msimamo wake kwa kumuunga mkono Sepp Blatter  kwenye uchaguzi wa Urais wa FIFA, Blatter alishinda lakini miezi kadhaa mbele ilibainika kuwa alikabiliwa na sakata kubwa la rushwa lililopelekea yeye kung’olewa kwenye nafasi yake.
Kwa hatua ya Malinzi kumuunga mkono Blatter, maswali mengi yalibaki miongoni mwa wadau ya Je Malinzi ni msafi? Je kama alikuwa akimpa sapoti Blatter, na rais huyo akangolewa kwa rushwa iwaje yeye awe msafi?
AWAWEKA NJIA PANDA STAND UNITED NA STAND UNITED COMPANY
TFF imelitolea maamuzi sakata la Stand United na lile kundi lililodai kuwa timu hiyo inatambulika kwa jina la Stand United Company lakini maamuzi ya TFF yamekuwa ni ya kusuasua kwa muda mrefu kwani walishindwa kufanya maamuzi ya hapo kwa hapo.
Matokeo ya kuchelewa yaliweka pande zote mbili njia panda, Stand United imekuwa ikifanya usajili kwa kususua bila ya kufahamu kama wanachokifanya ni sahihi.
Matokeo ya mgogoro huo ni timu hiyo kushindwa kusajili. Mnamo Julai 8, mwaka huu, Uongozi sahihi wa timu hiyo kupitia kwa msemaji wake, Deokaji Makomba alidai kuwa wameshindwa kusajili kwasababu ya kuvurugwa na kundi linalojiita Kampuni linaloongozwa na Mkurugenzi wao Dk Jonas Tiboroha.
Uchunguzi uliofanywa na Lete Raha umebaini kuwa akaunti ya Mfumo wa KIelektoniki wa Usajili yaani TMS ya klabu ya Stand imebadilishwa namba ya siri hivyo uongozi wa sasa wa timu hiyo umeshindwa kuingia kwenye mtandao huo kwa siku za karibuni.
Makomba alipoulizwa juu wa TMS kufungiwa alisema, “Tulikuwa tukiingia mara kwa mara kwenye akaunti yetu ya mfumo wa elekroniki ya usajili kwani tulikuwa na namba ya siri ya kufanya hivyo lakini ilivyoibuka mgogoro, inaonekana TFF walibadili namba ya siri.
“Tunashangazwa na hilo, kama TFF ilikuwa inatutambua ilikuwa inapaswa kuturuhusu sisi kuingia kwenye mtandao lakini hata nilipowasiliana na wahusika nimekuwa nikipigwa danadana, matokeo yake hata wale wanaojiita kampuni wamekuwa wakisajili licha ya kuwa TFF imedai haiwatambuhi,”alifafanua msemaji huyo.
Stand United halisi hivi karibuni ilimsajili mshambuliaji Adam Kingwande kutoka Kagera Sugar lakini siku mbili badaye wale wanaojiita Stand United Company walimpa mkataba mpya winga Haruna Chanongo ambaye Stand United halisi ilishatangaza kuachana naye.
Straika Paul Nonga ni moja ya wachezaji walioachwa njia panda na mgogoro huo huku mwenyewe akidai kuwa anachanganywa na mgogoro wa klabu hiyo na hivyo hawezi kusaini mpaka ple atakapoona mambo ni mazuri. Anasema, “ Nilifanya mazungumzo na Stand United halisi, pia Stand United Company ilinitafuta na tukazungumza lakini sielewi wapi sahihi. Mimi na rafiki zangu wengi tumekuwa tukikwama hivyo.”

No comments:

Post a Comment