Baada ya msanii kutoka Congo Koffi Olomide kukamatwa nchini Kenya, amekamatwa akiwa nyumbani kwake mjini Kinshasa.
Mwanamuziki huyo amekamatwa kwa agizo la ofisi ya mwendesha mashtaka.
Olomide alitimuliwa kutoka nchini Kenya baada ya video kuonekana akimpiga teke mnenguaji wa kike katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mapema asubuhi baada yake kuwasili.
Alipangiwa kutumbuiza mashabiki wake Bomas of Kenya siku ya Jumamosi lakini tamasha hiyo ikaahirishwa.
Alikamatwa Ijumaa usiku na maafisa wa polisi wa Kenya na siku iliyofuata asubuhi akaingizwa kwenye ndege na kurejeshwa Kinshasa.
Katika hatua nyingine, waandalizi wa tamasha ambalo Olomide alipangiwa kutumbuiza nchini Zambia pia walitangaza kufuta hafla hiyo kutokana na yaliyotokea Nairobi.
Mwanamuziki huyo, akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumapili, aliomba radhi mashabiki wake na hasa “wanawake na watoto”.
“Najutia sana yaliyotokea… kilikuwa ni kipindi kifupi cha wenda wazimu,” aliambia kituo cha televisheni cha taifa cha RTNC.
Baadaye, aliomba msamaha kutoka kwa raia wote wa DRC ambao huenda alihisi kwamba tabia yake iliwavunjia heshima.
Waziri wa masuala ya vijana na jinsia Kenya, Sicily Kariuki katika taarifa kwa vyombo vya habari baada ya video iliyoonyesha tukio hilo kusambaa, alipendekeza Olomide azuiwe daima kutembelea Kenya.
No comments:
Post a Comment