Yanga waridhia kutumia uwanja wa Uhuru, kukipiga na Mtibwa Oktoba 12
Keshokutwa Jumatano Oktoba 12, 2016 Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inatarajiwa kuendelea kwa michezo saba huku ule mchezo kati ya Young Africans ya Dar es Salaam dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro ukipangwa kufanyika Uwanja wa Uhuru jijini.Kwa mujibu wa Kanuni ya 6 kipendelea cha kwanza, Young Africans wametambulisha Uwanja wa Uhuru kama uwanja wa nyumbani kwa sasa baada ya kuleta maombi Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF) ambako baada ya kuyafanyia tathimini kwa mujibu kanuni hiyo ya sita, kipendelea cha sita, TFF imeiridhia klabu hiyo ya Mtaa wa Jangwani, kutumia uwanja wa Uhuru.Hatua hiyo inafuatia na Serikali – mmiliki wa viwanja vya Uhuru na Uwanja Mkuu wa Taifa, kuzuia klabu hiyo pamoja na ya Simba kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa michezo yao ya nyumbani kutokana na vurugu.Michezo mingine itakayopigwa Jumatano ni kati ya Mbeya City ya Mbeya na Simba ya Dar es Salaam, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya; Majimaji itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.Stand United itaikaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na katika mkoa huo huo Mwadui itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye dimba la Mwadui Complex huku timu pinzani za Mwanza ‘Mwanza Derby’ kati ya Mbao na Toto Africans itapigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo. Alhamisi Oktoba 13, 2016 Ruvu Shooting itacheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mabatini.
No comments:
Post a Comment