Wednesday, October 12, 2016

Maalim Seif kaandika barua kwenye Benki zote nchini kuzuia Profesa Lipumba kufungua akaunti kwa jina la Chama

Kukiwa bado kuna mkanganyiko wa kisiasa kwenye chama cha CUF sasa Katibu  Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, amemdhibiti mwenyekiti anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba kwa kuandika barua kwa benki zote ili kudhibiti ruzuku ya chama isipite kwenye mikono ya kiongozi huyo.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kumtambulisha Prof. Lipumba Benki ya NMB Tawi la Ilala akitaka apewe ushirikiano wa kufungua akaunti mpya ya chama.

Taarifa kutoka ndani ya CUF zinasema kuwa juzi Maalim Seif, aliandika barua kwa benki zote kuzuia hatua hiyo kwa kuweka zuio la mtu yeyote kufungua akaunti ya chama.

“Unajua hii vita si ya kitoto ni mapambano yaliyopo ndani ya CUF lakini yana nguvu kubwa kutoka katika kila pembe ya watu wanaochukia upinzani. Na pia wapo hata viongozi wakubwa wa dola ambao kila siku wamekuwa wakifanya kazi ya kuivuruga CUF.

“Walitegemea lakini tangu jana (juzi) Katibu Mkuu ameziandikia barua benki zote nchini kuzuia mpango wa Msajili kutaka kuchepusha ruzuku ya chama na kwenda katika mikono ya Lipumba na sasa nakala yake imepelekwa kwa Msajili wa Vyama,” alisema mtoa habari wetu.

Hatua ya Profesa Lipumba kufungua akaunti inatokana na barua aliyopewa na Msajili wa Vyama vya Siasa ya Oktoba 6, mwaka huu iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kwenda kwa Meneja wa Benki NMB Tawi la Ilala.

Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba HA.322/362/14/104  inamtambulisha Profesa Lipumba kutakiwa kufungua akaunti mpya ya The Civic United Front (CUF).

Siri ya Profesa Lipumba kutaka kufungua akaunti mpya yenye jina la Chama cha Wananchi CUF inadaiwa kutolewa na watumishi wa benki wa tawi hilo.

Prof. Lipumba ni Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, huku chama chake kikiwa tayari kimemfukuza uanachama.

Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kupitia Sisty Nyahoza ilinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikikiri kumtambulisha Profesa Lipumba kwa Benki ya NMB ili aweze kufungua akaunti hiyo, hata hivyo ikikana kujua matumizi ya akaunti hiyo.

No comments:

Post a Comment