Mbele ya Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza anayesikiliza shauri hilo la kupinga matokeo yaliyompa ushindi Bulaya, Wakili Lissu alimbana Wasira ambaye ni shahidi wa upande wa wadai kuwa aithibitishie mahakama madai yake kuwa mteja wake hakujaza fomu ya kuonyesha gharama za kampeni kulingana na sheria ya uchaguzi.
Akijibu hoja hiyo, Wasira aliiambia mahakama kuwa licha ya kutokuwa na barua rasmi kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuthibitisha madai hayo, ukimya wa upande wa utetezi kuhusu suala hilo unathibitisha kuwa huenda Bulaya hakujaza fomu hiyo.
Lissu alimtaka pia Wasira aieleze mahakama kwanini Mahakama ya Rufani ilimfungia kushiriki uchaguzi kwa kuchaguliwa wala kupiga kura kwa kipindi cha miaka mitano baada ya matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mwaka 1995 kubatilishwa.
Sehemu ya mahojiano kati ya Wakili na shahidi huyo katika shauri hilo namba moja la mwaka 2015 lililofunguliwa na Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila yalikuwa hivi:
Lissu: Naomba umueleze Jaji, Mahakama ya Rufani ilikufungia kugombea miaka mitano kwanini kama haukuhusika na rushwa?
Wasira: Mahakama ya Rufani Tanzania ilifanya uamuzi huo baada ya kupokea rufaa na kutumia kigezo cha mazingira ya rushwa kama ilivyoamriwa na Mahakama Kuu na sikuwa na sehemu ya kukata rufaa maana ndiyo ilikuwa sehemu ya mwisho.
Lissu: Hivyo Mahakama hiyo imesema imeridhika na matokeo ya rushwa na kukufungia miaka mitano?
Wasira: Mahakama iliridhika na azimio la Jaji Lugakingira kuwa kulikuwapo na mazingira ya rushwa ....si kweli kwamba nilitoa rushwa na Mahakama haikusema hivyo bali ni mazingira.
Awali, akiongozwa na wakili Constantine Mutalemwa anayewawakilisha walalamikaji wanne katika shauri hilo, Wasira aliieleza mahakama kuwa licha ya Bulaya kutangazwa kuwa mshindi, ushindi wake haukuwa halali kwa sababu ulitokana na kuwapo kwa wapigakura hewa.
Alidai awali idadi ya wapigakura kwa mujibu wa maelezo ya wadau wa uchaguzi walikuwa 69,396 lakini ikaongezeka hadi kufikia 164, 794, huku vituo vya kupigia kura vikiongezeka kutoka 190 hadi 199. Aliieleza mahakama kuwa pamoja na kasoro hiyo, mchakato wa uchaguzi jimbo hilo uligubikwa na kasoro kadhaa ikiwamo wafuasi wa Chadema kuendelea na kampeni hadi siku ya kupiga kura kinyume cha sheria.
Alimueleza Jaji Chocha awali alipata taarifa za kampeni kuendelea katika vituo vya kupiga kura kutoka kwa wafuasi wake na akajiridhisha kwa kutembelea baadhi ya vituo. Aliiomba Mahakamani kubatilisha matokeo na kuamuru uchaguzi mwingine akidai uliopita haukuwa huru na haki.
Source: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment