Sunday, October 9, 2016

ACT Wazalendo na miaka 50 ya azimio la Arusha..

Chama cha ACT Wazalendo kimeazimia kufanya maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la Arusha Februari mwakani pamoja na kueleza mafanikio na changamoto zake.

Maazimio hayo yametokana na mkutano wake wa kwanza wa kisera, uliofanyika tangu Uchaguzi Mkuu wa 2015 umalizike.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Ofisa Habari wa ACT Wazalendo, Abdallah Khamis, ilieleza kuwa maadhimisho hayo, yatatanguliwa na Halmashauri Kuu ya chama katika eneo ambalo Chama cha TANU kilifanya mkutano uliozaa Azimio la Arusha mwaka 1967.

Khamis alisema katika maadhimisho hayo, imeshauriwa wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wawepo kwa ajili ya kujadili mafanikio na changamoto za Azimio la Arusha katika miaka 25 ya kutekelezwa kwake na madhara yake tangu lizikwe huko Zanzibar mwaka 1992.

Aidha, ACT imeazimia mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uanze sasa kwa kufanya marekebisho ya sheria ya kura ya maoni na sheria ya mchakato wa Katiba.

Alisema chama hicho kimemuomba Rais John Magufuli, kuunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kupitia Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba na kuitisha mkutano mkuu wa kikatiba wa wananchi ili kupitisha katiba pendekezwa na kwenda kwenye kura za maoni.

No comments:

Post a Comment