Tuesday, October 11, 2016

Kuhusu uwepo wa dawa nchini Wizara ya Afya yatoa ufafanuzi

Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa katika baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii vikizungumzia hali ya dawa nchini hasa kufuatia taarifa zilizotolewa na taasisi ya kiraia na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.
Taarifa hizo zilidai kwamba katika kipindi hiki kuna upungufu mkubwa wa dawa katika bohari kuu ya dawa , Hivyo, kusababisha kukosekana kwa dawa katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
Taarifa hizi si sahihi na zinalenga kupotosha umma na kuwatia wananchi wasiwasi. Napenda kuwathibitishia wananchi kuwa Afya ni suala la kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Hivyo, ningependa kutoa ufafanuzi kwa wananchi katika masuala yafuatayo; –
Hali ya Upatikanaji wa dawaHali ya upatikanaji wa dawa kwa sasa iko vizuri. Dawa muhimu zinazohitajika  sana nchini zinapatikana kwenye maghala ya Bohari ya Dawa (MSD). Mfano kwa upande wa dawa za antibiotics tuna Amoxycillin, Ciprofloxacin, Cotrimoxazole na Doxycycline. Kwa upande wa dawa za maumivu – tunazo za kutosha kama vile paracetamol, asprin na diclofenac.
Pia tuna dawa za kutosha za malaria, Kifua Kikuu, ukoma na dawa za kufubaza makali ya UKIMWI (ARVs). Kwa upande wa chanjo za watoto na wajawazito, ni kweli kulikuwa na uhaba nchini kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita. 
Hata hivyo, wiki iliyopita Serikali imenunua na kupokea dozi milioni 2 za chanjo ya Kifua Kikuu (BCG), dozi milioni 1.2 za Polio na dozi milioni za Polio. Chanjo hizi zinasambazwa katika vituo vya afya nchini.
Dawa nyingine zitaendelea kupatikana katika Bohari kuu ya Dawa kwa kuwa tumeagiza dawa za kutosha kutoka kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi. 
Aidha, kiasi kikubwa cha dawa zinazowasili Bohari kuu ya Dawa zikifika zinapelekwa kwenye Kanda nane za MSD pamoja na vituo viwili vya Mauzo kwa ajili ya kuwasambazia wateja walioagiza. 
Hivyo, kipimo cha upatikanaji wa dawa si kuangalia katika maghala ya Bohari ya Dawa peke yake bali pia katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Ili kuondoa mlolongo wa manunuzi ya dawa, tunapenda kuwataarifu kuwa Bohari kuu ya Dawa imepanua wigo wa upatikanaji wa dawa kwa sasa kwa kutumia mikataba ya muda mrefu (miaka miwili) na washitiri wa ziada wa ndani (Prime Vendors) ili kuhakikisha dawa zinapokosekana MSD zinapatikana kwa haraka kwa Washitiri wa ndani waliothibitishwa katika kila mkoa.
Katika muktadha huo huo, Bohari ya Dawa imefungua maduka ya ziada kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa dawa zaidi ya aina 600 kupitia mfumo wa maduka katika mahospitali kama vile Muhimbili, Mbeya na Arusha.
Bajeti ya dharura kwa ajili ya dawaNi muhimu wananchi wakajua kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya manunuzi ya dawa katika mwaka wa fedha 2016/17 zinatosha kuhudumia mahitaji ya dawa kwa mwaka mzima. Hivyo hakuna sababu ya kuwa na bajeti ya dharura.
Niwakumbushe bajeti zilizotengwa kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba katika miaka michache iliyopita mpaka hivi sasa, kama ifuatavyo: -.
Mwaka 2011/2012 bajeti iliyotengwa ilikuwa shilingi Bilioni 23.7
Mwaka 2012/2013 bajeti ilikuwa shilingi Bilioni 34
Mwaka 2013/2014 ilikuwa shilingi Bilioni 34
Mwaka 2014/2015 ilikuwa shilingi Bilioni 60
Mwaka 2015/2016 ni shilingi Bilioni 30
Na mwaka huu 2016/17 ni shilingi Bilioni 251.5
Mkakati wa Wizara kwa sasa ni kuhakikisha kuwa fedha hizo zinapatikana kwa wakati kutoka Hazina kulingana na makusanyo ya nchi.
Vilevile ieleweke kwamba tayari serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 20 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17,  kwenda Bohari kuu ya Dawa kwa ajili ya ununuzi wa dawa na chanjo. Hali hii inathibitisha kuwa suala la upatikanaji wa dawa ni la kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya tano.
Kulipa Deni la Bohari ya Dawa (MSD)Napenda kuwafahamisha kuwa Serikali imedhamiria kulipa deni lote la Bohari ya Dawa (MSD) ambapo katika mwaka huu wa fedha 2016/17 tayari Bilioni 85 imekwishatenga kwa ajili ya kulipa deni hilo.Jambo ambalo halijawahi kutokea huko nyuma. Kulipwa kwa deni hilo kutasaidia kuhuisha mtaji wa MSD (revolving fund) na hivyo kuiwezesha MSD kuwa na dawa na vifaa tiba kwa kiwango kikubwa.
Aidha serikali imekwisha kuviagiza vituo vyote vinavyotoa huduma za Afya kupitia Halmashauri zao, kuhakikisha zinakuwa na fedha ya mzunguko kwa ajili ya kununulia dawa (revolving fund) na hivyo kupata dawa kwa kulipa fedha taslimu kutoka Bohari ya Dawa badala ya kukopa.
Fedha hizo zitapatika kutoka kwenye vyanzo vyao vingine vya mapato kama vile Bima ya Afya (NHIF, CHF) na gharama wanazochangia wananchi katika kupata huduma. Hii itawezesha kutoendelea kukuza deni kutoka Bohari ya Dawa na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati wote.
MSD Kupata MshindaniKatika mwaka 2015, Serikali ilimpa kazi mshauri mwelekezi wa kampuni ya ushauri iliyobobea kimataifa ya Deloitte ya kulitazama jambo hili kwa ajili ya kuifanyia tathmini MSD pamoja na mambo mengine ikiwemo kuangalia suala ya kutafutiwa mshindani katika manunuzi na usambazaji wa dawa.
Napenda kuwajulisha kuwa tathmini hiyo ilionyesha kuwa MSD kutafutiwa mshindani itakuwa ni kuongeza gharama kubwa kwa serikali kutokana na kurudufisha (duplication) majukumu. 
Pia ilibainika kuwa suala la dawa ni muhimu, hivyo Serikali haiwezi kuliacha kwenye mikono ya watu binafsi.Jambo ambalo lilipendekezwa ni kuifanyia maboresha makubwa MSD ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Utekelezaji wa mapendekezo hayo tayari umeshaanza.
Nchi ambazo zinaiuzia dawa na vifaa tiba MSDMSD inaagiza dawa na vifaa tiba nje ya nchi zaidi ya asilimia 80 kwa sababu viwanda vilivyoko ndani ya nchi havikidhi mahitaji ya nchi kwa ubora na kiasi. Hivyo, MSD hununua dawa na vifaa tiba kutoka nchi za India, China, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Ujerumani, Marekani, Ufaransa na sehemu nyingine duniani.
Kwa mfano, tuna dawa zaidi ya aina  nne ambazo zinanunuliwa kutoka Kenya (Dawa ya kutibu malaria kwa akina mama wajawazito ijulikanayo kama Sulfadoxine Pyrimethamine (SP), dawa ya kutibu magonjwa ya maambukizi ya Cotrimoxazole  ya watu wazima na watoto pamoja, Amoxicilline  na Paracetamol ya maji kwa ajili ya watoto.
Ikumbukwe kuwa MSD hununua dawa hizi kupitia mchakato wa zabuni, ikiwa baadhi ya vigezo ni kuangalia usajili wa dawa nchini pamoja na ushindani wa bei. Hata hivyo, ili kukuza viwanda vya ndani, watengenezaji wa dawa wa ndani hupewa hadi 15% ya upendeleo katika mchakato wa tathmini ya zabuni dhidi ya dawa zinazotoka nje ya nchi (Domestic preference).
Kwa upande mwingine mkakati wa serikali sio kuendelea kutegemea dawa kutoka nje ya nchi, kwani kwa kufanya hivi uchumi wa nchi hautakuwa. hivyo basi serikali iko katika hatua za mwisho za utaratibu wa kuwakaribisha wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha dawa kuwekeza nchini kwa mpango wa kuwashirikisha wadau wengine katika masuala ya dawa  (PPP).
HitimishoWizara ya afya inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa itasimammia ipasavyo utapatinaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba nchini kwa wakati na kwa bei nafuu kwa kuwa Sera ya afya inawataka wananchi kuchangia huduma.
Aidha vituo vya kutolea huduma za Afya vinahimizwa kupeleka mahitaji na maoteo yao ya dawa kwa wakati badala ya kusubiri hadi dawa zote muhimu zimeisha kabisa katika vituo vyao. Pia wanakumbusha kulipa madeni wanayodai na bohari ya dawa sambamba na kuhakikisha fedha inayopatikana katika shughuli za utoaji huduma inatumika kwa ajili ya dawa, vifaa na vifaa tiba.
 Ili kuondoa vikwazo kwa wananchi katika kupata dawa na huduma za afya kwa ujumla wananchi wanahimizwa kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya kwani hakuna anayejua leo hama kesho ataugua na Magonjwa hayapigi hodi na wakati mwingine yanakukuta hauna  akiba ya fedha, ila ukiwa na bima wakati wowote unapata matibabu.
Mwisho, Wizara itaendelea kuhakikisha kuwa kuna dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara vya kutosha kwenye vituo vya umma vya kutolea huduma za Afya nchini

No comments:

Post a Comment