DK MASHINJI- CHADEMA TUNAJIPANGA KUJENGA OFISI ZETU
DK. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema chama chake kimejipanga kutekeleza mpango wa ujenzi wa ofisi za chama kuanzia ngazi ya taifa mpaka katika majimbo, kwa kushirikiana na wanachama wake.Dk. Mashinji amesema mpango huo utatekelezwa kama ilivyoagizwa na Baraza Kuu la chama hicho.“Baraza Kuu la Chadema liliagiza viongozi wa majimbo na wilaya waanze kuchukua hatua za awali ili kutekeleza mpango wa ujenzi wa ofisi za chama, sisi tutawaunga mkono kama tulivyoanza kufanya katika Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani,” amesema.Dk. Mashinji na Waziri Mkuu Mstaafu, Federick Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, walifanya ziara ya kufungua matawi ya chama hicho wilayani Mkuranga siku ya jana huku pia wakiendesha harambee ya kukusanya fedha za ujenzi wa ofisi.Jumla ya Sh. 12 milioni zilipatikana katika harambee hiyo ili kufanikisha ujenzi wa ofisi za Chadema Wilaya ya Mkuranga. Dk. Mashinji amesema zoezi hilo litaendelea katika mikoa na majimbo yote na kwamba viongozi wa majimbo waanze kuchukua hatua za awali.“Sisi hatuna rasilimali za kutosha kuweza kujenga ofisi katika majimbo, wilaya na mikoa yote ndani ya muda mfupi, lakini tuna mtaji wa watu wanaokipenda chama hiki, kwahiyo tutautumia mtaji huo kuhakikisha tunajenga ofisi za chama katika maeneo mbalimbali,” amesema.Kuhusu ofisi za Makao Makuu ya Chadema, Dk. Mashinji amesema kuwa, chama hicho kimejiwekea mpango wa kujenga ofisi hizo pia.“Tumejipanga kwa ujenzi wa Makao Makuu pia, tunaamini mambo yataenda vyema na tutatekeleza mikakati tuliyojiwekea, ndiyo maana tunaomba viongozi na wanachama wetu katika ngazi za chini waanze kuchukua hatua za awali kama walivyoanza kule Mkuranga,” amesema.
No comments:
Post a Comment