Saturday, October 8, 2016

Hapa ni habari kamili ya kifo cha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) Dodoma

Kuna taarifa za majonzi za kifo cha Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake Tanzania UWT Mkoa wa Dododma ambapo chanzo cha kifo hicho kilikua kinaleta utata.

Mashuhuda  wa ajali wamesema alikufa kutokana na kushindwa kupewa msaada kwa haraka.

Walisema baada ya ajali walisikia sauti za watu wakilia kuomba msaada lakini ilichukua muda wa sasa tatu ndipo walipopata msaada wa kuokolewa kutokana na ukosefu wa vifaa vya uokoaji.

Juzi katika eneo la Emmaus mkoani hapa ilitokea ajali ya gari la Toyota Noah na lori ambayo ilichukua maisha ya Mwenyekiti huyo na watu wengine watatu kujeruhiwa. 

Mmoja wa mashuhuda hao Amri Juma alisema alisikia sauti za wanawake wakiomba msaada ili waweze kuokolewa.

“Ni jambo la kusikitisha kuona zaidi ya saa tatu hakuna vifaa vya uokoaji vilivyokuwa vimefika kwa ajili ya uokoaji, ajali ilitokea saa nane mchana lakini mpaka saa 11 jioni ndio watu wanakuja kutolewa.

‘’‘Breakdown moja ilipofika ilishindwa kunyanyua lori, ilipofika ya pili ilishindwa, hali inayoonesha kuna uhaba wa vifaa hivyo mamlaka husika zijipange kuwa na vifaa vya uokoaji."

 Juma alisema Dodoma imeanza kuandaliwa kuwa makao makuu ya nchi hivyo wakati umefika wa kuanza kujengewa uwezo wa kuwa na vifaa vya kisasa vya uokoaji. 

Katibu wa UWT Mkoa wa Dodoma, Kaundime Kasase, akizungumzia kifo hicho alisema;

“imeniuma sana na bado inaniuma, sina hata la kusema kwani nimefanya naye kazi kwa ukaribu, alikuwa mtu anayependa viongozi wake wote."

Mtoto aliyekuwa ndani ya gari hilo, Dearest Mabuba (8) alisema;“Tulikuwa tumetoka kwenye birthday (siku ya kuzaliwa) yangu ndipo gari likapata ajali, mama yangu Annastazia Amandus ambaye alikuwa akiendesha gari hilo akaumia kichwani na dada akachanika kwenye kiwiko,” alisema.

Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jaffari Mwanyemba alisema wamempoteza mtu muhimu.

“Alikuwa akijichanganya kila mahali, tumepoteza mtu muhimu tuige mazuri yake”. 

Mbunge wa Viti Maalumu na Mwenyekiti mstaafu wa UWT Mkoa wa Dodoma, Fatma Tawfiq alisema;

“Mwenyezi Mungu ndiye alikuwa akifahamu siri hii. “Ni jambo la kushtukiza sana tumuombee Mungu amuweke mahali pema peponi,”alisema.

Hata hivyo kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Dodoma, Marson Mwakyoma alisema walifika eneo la tukio dakika 10 baada ya ajali hiyo kutokea.

“Si lazima askari avae sare tulifika mapema na vikosi vingine vya uokoaji vilikuja kwa wakati, nadhani kitu muhimu kinachotakiwa kufanyika ni kuimarisha vifaa vya uokoaji,” alisema.

Chanzo | Mpekuzi

No comments:

Post a Comment