Sunday, October 9, 2016

Babu Seya, Papii Watuma Ujumbe Mzito Kwa JPM!


Kwa Wabongo walio wengi, majina ya Nguza Viking ‘Babu Seya’ na Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ siyo mageni. Wao ni wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha ndani ya Gereza la Ukonga, Dar baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kulawiti na kunajisi watoto 10.


Tangu kufungwa kwao, mwaka 2004, miaka 12 iliyopita, mengi yamesemwa, mengi yameandikwa, lakini wenyewe hawajawahi kufungua vinywa kusema lolote, hivyo kwa mara ya kwanza, Septemba 3, mwaka huu, Risasi Mchanganyiko, limekutana nao ndani ya gereza hilo na kufanya nao mahojiano yaliyochukua dakika 55.

ILIKUWAJE?
Septemba 2, mwaka huu, Risasi Mchanganyiko lilipata taarifa kwamba, wafungwa hao waliandika barua kwa Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ wakiomba msamaha kutoka kwake ili waachiwe huru.
Ili kuweka sawa mzani wa habari, Risasi Mchanganyiko lilimpigia simu Mkuu wa Gereza la Ukonga, ACP Stephen Mwaisabila na kumuuliza kuhusu uwepo wa madai hayo ambapo alisema:
“Hakuna kitu kama hicho. Hivi ni kwa nini baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika habari za hawa watu wawili bila ukweli wowote?”


Risasi Mchanganyiko: “Sasa ukweli ni upi kamanda?”
ACP Mwaisabila: “Ukweli ni kwamba si kweli, hawajaandika barua. Mimi nadhani nyie mngekuja hapa ili muongee nao mbele yangu, muwasikie wenyewe. Maana muda mrefu nasoma kwenye magazeti habari za hawa watu ambazo si za kweli. Wengine wanaandika wameachiwa, wengine wanasema Babu Seya amelazwa yu hoi. Njooni muone kama kweli yupo hoi.”
Risasi Mchanganyiko: “Itakuwa vizuri sana kamanda. Ili tuzungumze nao mambo mengine ambapo Watanzania wakisoma, ukweli na uongo utajulikana.”
ACP Mwasabila: “Sawasawa.”seyaaaa-7…Wakiwa katika sura ya majonzi.

NDANI YA GEREZA LA UKONGA
Ndani ya gereza hilo, maisha yalikuwa yakiendelea. Wafungwa walionekana kufanya shughuli zao za kila siku. Hakukuwa na dalili zozote za vurugu wala uvunjifu wa amani. Wafungwa walionekana wanaishi maisha ya maelewano na askari wao.

BABU SEYA, PAPII WAITWA

Baada ya salamu na mkuu wa gereza, askari mmoja alitumwa kwenda kuwaita wafungwa hao. Ndani ya dakika kumi, wakafika na kupeana salamu na Risasi Mchanganyiko.

BAADA YA SALAMU SASA

Baada ya salamu, Risasi Mchanganyiko lilianza maswali papohapo.
Risasi: “Tulipata taarifa kwamba, mmeandika barua kwa Rais Magufuli kuomba msamaha kutoka kwake. Hii habari imeenea mtandaoni. Hebu tuambieni, ipoje?
Babu Seya: “Iko hivi, sisi…”


Papii: (akadakia yeye, baba yake akanyamaza) “ngoja niseme mimi. Ukweli ni kwamba, barua niliandika mimi mwaka 2010. Ilikwenda kwa Rais Kikwete (Jakaya, wakati huo). Lakini tangu pale sijawahi kuandika tena barua. Hiyo inayosambaa mtandaoni ni ileile inajirudia. Kwa Magufuli hatujawahi kuandika barua.”

KUHUSU RUFAA YAO
Risasi: “Sawa. Kwa nafasi hii tungependa kuzungumza na nyie mambo mbalimbali ambayo hamjawahi kuyasema tangu mmeingia gerezani. Hebu tuanze na kesi yenu. Kuna wakati ilisemekana mmekata rufaa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika yenye makao yake Arusha, mkipinga kifungo. Je, nini kinaendelea?”
Papii: “Ni kweli. Ila ilichotakiwa ni wao baada ya sisi kupeleka hati yetu, walitakiwa kuja kutuhoji ili wajue tulichoandika ni sawa au kuna ya kuongezea. Lakini hawajatokea.”


WANAAMINI WATATOKA?
Risasi: Kwako Babu Seya. Je, mnaamini kuwa iko siku moja mtatoka gerezani?”
Babu Seya: “Mimi naamini kwa haki ya Mungu iko siku lazima. Nasema hivi kwa sababu, Mungu ndiye anayejua ukweli wa kesi tuliyofungiwa. Anajua nini kilitendeka.”
Papi Kocha: (anaunga mkono maneno ya baba yake kwa kutingisha kichwa).

BABU SEYA AUTAJA WIMBO WA SEYA
Risasi: “Kwani kwako Babu Seya, unataka kusema kuna namna katika ile kesi yenu? Hiyo namna iko wapi?”
Babu Seya: “Chanzo cha yote yale ni Wimbo wa Seya niliouimba mimi na mtoto wangu (Papii). Ule Seya wa Mivano. Pale ndipo pana chanzo, lakini siwezi kusema nini kilitokea, siko tayari kusema.”

SIKU YA KWANZA GEREZANI ILIKUAJE?
Risasi: “Hivi siku yenu ya kwanza kuingia hapa gerezani ilikuaje? Mlilia kwa kiasi gani?”
Babu Seya: “Wala! Tulimwamini Mungu. Tulijua Mungu ana makusudi yake na iko siku itajulikana ukweli umesimamia wapi.”

MAISHA YA GEREZANI
Risasi: “Maisha yenu hapa jela yakoje? Maana tukiwaangalia tunawaona mpo fiti sana.”
Babu Seya: “Kama hivi, tunaendelea vizuri sana. Tumezoea na hakuna unyanyasaji wowote.”

KUNA UGONJWA UMEWAPATA GEREZANI?
Risasi: “Kumekuwa na madai kwamba, wewe Babu Seya unaumwa. Wakati mwingine ikadaiwa upo hoi. Je, kuna ugonjwa umekupata ukiwa hapa au mwanao?
Papii: (anatingisha kichwa kukataa).
Babu Seya: “Mimi niliumwa, nikaenda kupimwa na kugundulika nina diabetes (kisukari). Ni kama miaka minne iliyopita (2012).
“Ninapoonekana Muhimbili (hospitali), huwa nakwenda kliniki. Kwa hiyo siyo kweli kwamba nakuwa hoi. Kisukari ni ugonjwa kama magonjwa mengine na nimeupata kama wanavyoweza kuupata watu wengine ambao hawapo gerezani.”

WAMESHIKA IMANI GANI GEREZANI?
Risasi: “Wengi wakiingia gerezani hubadili imani. Wapo ambao huamua kuokoka. Nyie je, tangu mmefika mmebadili madhehebu?”
Papii: “Hapana, sisi tuko na imani yetu ileile ya Romani Katoliki. Tulipokuwa nje, kanisa letu lilikuwa pale Sinza, Shule ya Msingi Mashujaa kwa mbele (Barabara ya Hoteli ya Lion).”
Risasi: “Tangu mmekutwa na hatia na kutupwa huku jela, viongozi wenu wa dini wameshakuja kuwajulia hali?”
Papii: “Hapana.”



BEBU SEYA BENDI ALIMUACHIA NANI?
Risasi: “Tunajua Babu Seya ulikuwa na bendi yako ya muziki, Achigo Band na ulikuwa ukipiga pale Lion Hotel. Je, ulimwachia nani?”
Babu Seya: “Ile nilimwachia mwanangu mkubwa.”
Risasi: “Mbangu?”
Babu Seya: “Hapana, kaka yake.”

BABU SEYA ANA MKE?
Risasi: “Babu Seya umeacha mke uraiani?”
Babu Seya: (anasikitika) “Hapana, mke wangu alifariki dunia kabla mimi sijakumbwa na ile kesi.”

LAKINI UKWELI NI UPI, WALIBAKA?
Risasi: “Msamaha wa binadamu ni jambo muhimu sana. Hata Mungu anauona na unaposema ukweli na kukiri kile ulichokifanya, anaweza kukusamahe. Maana kama ni kufungwa tayari mpo kifungoni, hakuna sababu ya kudanganya tena. Je, ukweli wenu ni upi? Ni kweli mlibaka???”
Kutokana na ufinyu wa nafasi, mahojiano na Babu Seya na Papii Kocha yataendelea kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi, usikose.

LAKINI UKWELI NI UPI, WALIBAKA?
Risasi: “Msamaha wa binadamu ni jambo muhimu sana. Hata Mungu anauona na unaposema ukweli na kukiri kile ulichokifanya, anaweza kukusamahe. Maana kama ni kufungwa tayari mpo kifungoni, hakuna sababu ya kudanganya tena. Je, ukweli wenu ni upi? Ni kweli mlibaka?”

Kutokana na ufinyu wa nafasi, mahojiano hayo yalikatwa hapo bila wao kujibu. Sasa sikia majibu yao…
Babu Seya: “Kusema ukweli kwa haki ya Mungu nakuapia, mimi wala dogo huyu (Papii) hakuna anayehusika na yale madai. Hata siku ya kukamatwa, mimi nilikuwa nyumbani wakati ule pale Sinza, nikashangaa navamiwa, naambiwa nimebaka wale watoto. Huyu dogo (Papii) yeye alikuwa ametoka Arusha, akaunganishwa kwamba naye alikuwemo.
“Ndiyo maana nikasema kwamba ule Wimbo wa Seya wa Mivano pana kitu. Lakini sikisemi. Wale watoto mimi hata kuwajua siwajui maskini ya Mungu.”
Risasi: “Kwa hiyo hamkubaka?”
Babu Seya: “Kwa vile hukumu imeshapita, mahakama ikatuona tuna hatia, hakuna namna ambayo tunaweza kusema zaidi ya kukiri kwamba tulifanya kwa sababu tulikutwa na hatia…
Papii: (akadakia) “Maana hata tukisema hatukubaka, watu watatuuliza kwa nini sasa tuko gerezani? Mtu ukishahukumiwa tafsiri yake ulitenda kosa na ndiyo maana ulikutwa na hatia hata kama hukufanya lile kosa.”

WAWAOMBA WATANZANIA WAWASAMEHE
Risasi: “Kwa maana hiyo mnapoyazungumza hayo, mnawaambia nini Watanzania?”
Babu Seya: “Tunawaomba watusamehe kwa yote yaliyotokea na watuombee kwa Mungu siku moja tutoke gerezani ili kuungana katika ujenzi wa taifa.”

WAKITOKA GAREZANI WAMEPANGA KUFANYA NINI?
Risasi: “Ni kawaida kwa watu waliofungwa wakitoka gerezani kubadili mstari wa maisha. Wengine huamua kumtumikia Mungu, wengine hufanya shughuli yoyote tofauti na ile ya awali. Je, nyie ikitokea mmetoka jela, mmepanga kufanya shughuli gani?”
Babu Seya: “Kwanza ikitokea tukaachiwa huru tutachanganyikiwa. Hivyo hatujawahi kupanga cha kufanya. Maana tukisema tukitoka tutamtangaza Mungu, watu watasema tumechanganyikiwa (kicheko, Papii naye kicheko).
“Lakini tukisema tuendelee na muziki, pia watu watasema tunarudia mambo yetu. Kwa hiyo tutaangalia cha kufanya wakati ukifika.”
Risasi: “Babu Seya umesikika ukisema uliishi Sinza. Kwani kwa sasa maskani ya familia yako ni wapi?”
Babu Seya: “Yapo Kimara. Pale Sinza niliuza nyumba baada ya ndugu kunishauri ili nibadilishe mazingira.”
Risasi: “Familia yako ikoje sasa?”
Babu Seya: “Familia haiko sawa kwani roho ni mimi na ndiyo niko gerezani. Kwa hiyo familia haiko sawasawa maana roho haipo (kicheko).”

UJUMBE WAO MZITO KWA MAGUFULI NI HUU
Risasi: “Mlisema kuwa, mliwahi kuandika barua kwa Jakaya Kikwete kabla ya Rais Magufuli. Je, kwa Magufuli mnampa ujumbe gani?”
Babu Seya: “Sisi kwa nafasi hii ya leo, tunamuomba sanasana Rais Magufuli aitishe faili la kesi yetu (huku Papii akitingisha kichwa kukubaliana na maneno ya baba yake). Asome mwenyewe mwanzo hadi mwisho, aone ukweli uko wapi! Lazima atabaini ukweli kwamba kufungwa kwetu kulitokana na nini!
“Lakini naamini kwamba, Mungu hawezi kuacha jambo ambalo si la kweli liendelee kujulikana si la kweli kwa muda wote, lazima kuna siku atainua nguvu zake na ukweli utajulikana. ”

IKITOKEA HAKUNA NAMNA YA KUTOKA
Risasi: “Je, endapo itatokea njia zote za kutoka jela zimeshindikana, mtafanya nini?”
Babu Seya: “Tutamshukuru Mungu na kumwachia yeye kila kitu. Kwani lazima atakuwa na makusudi yake.”

KUTOKA MOYONI KWA BABU SEYA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Babu Seya alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, anamwomba Mungu ikiwezekana hata kama yeye hatatoka, basi mwanaye, Papii atoke ili akafanye maisha yake.
“Unajua mimi umri umekwenda. Sasa huyu dogo (Papii) bado kijana. Alikuwa ana malengo yake, yote yamepotea. Mimi hata nikibaki basi Mungu asaidie yeye atoke,” alisema Babu Seya.

KUNA MWENYE CHEO?
Risasi liliwashuhudia wote wakiwa na mikanda kiunoni ambayo kwa mfungwa, inaashiria ni nyapara (msimamizi wa wafungwa).

BABU SEYA ALITABIRI TETEMEKO LA BUKOBA
Katika kusimulia zaidi maisha ya gerezani, Babu Seya alisema amekuwa akisali sana kiasi kwamba, wakati mwingine Mungu humwonesha mambo yajayo.
“Siku tatu kabla ya tetemeko la ardhi kule Bukoba, mimi nililala nikasikia sauti ikiniambia; ‘fungua macho uangalie’. Kufungua hivi nikaona ardhi inatetemeka. Nikalala tena, nikaambiwa tena.
“Nikamfuata dogo (Papii) na wenzake, nikawaambia kutatokea tetemeko la ardhi. Kweli, baada ya siku tatu tukasikia Bukoba kumetokea tetemeko na limesababisha maafa.”

AOMBA KUANDALIWA TAMASHA
“Kwa hiyo kutokana na tukio la tetemeko, mimi naomba kama inawezekana serikali ituandalie tamasha mimi na dogo tupige ili kuwachangia waathirika wa tetemeko,” alisema Babu Seya.

WANAMUZIKI WANAKWENDA KUWATEMBELEA?
Risasi: “Tangu mmefungwa jela, kuna wanamuziki wanakuja kuwatembelea?”
Babu Seya: “Ilikuwa zamani, siku hizi wameacha. Ila mwanamuziki anayekuja sana mpaka sasa ni King Kiki (Kikumbi Mwanza Mpango).

PAPII KOCHA ANAMMISI NANI?
Risasi: “Kwako Papii. Unaweza kusema unawamisi akina nani kuwepo kwako jela?”
Papii: “Nawamisi mashabiki wangu wote. Pia, nawamisi Bongo Fleva na Bongo Muvi. Nammisi mwanamke niliyezaa naye mtoto mmoja, anaitwa Mariam.
“Lakini namuomba Rais Magufuli aendelee kufanya mambo yake vizuri kama tunavyosikia maana yakiharibika na sisi huku gerezani mambo yatakuwa mabaya.”
Risasi: “Basi tunashukuru sana, tunawaombea kwa Mungu.”
Babu Seya: “Na sisi tunashukuru sana, muende salama na mzidi kutuombea.”

Waandishi: Oscar Ndauka na Elvan Stambuli/GPL.

No comments:

Post a Comment