Friday, October 14, 2016

Mwinyi asema ana wasiwasi na Tanzania tuliyopo

Ikiwa Tanzania leo inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema ana wasiwasi na Taifa la sasa kwani halina uadilifu, aliotujengea Mwalimu Nyerere.Mwinyi aliyerithi mikoba ya urais kutoka kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1985, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mdahalo wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuzindua kitabu cha ‘Selective works of Mwalimu Nyerere’, kilichotafsiriwa na wasomi kutoka China.
Mdahalo huo uliandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikishirikiana na Ubalozi wa China na Asasi ya Urafiki kati ya Tanzania na China. Mwalimu Nyerere aliyeitawala Tanzania kwa takribani miaka 24, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 kwenye Hospitali ya St Thomas jijini London nchini Uingereza ambako alikuwa akitibiwa maradhi ya saratani ya damu.
Aliiongoza Tanzania kwa uadilifu mkubwa akisimamia misingi ya haki, umoja, mshikamano, kupiga vita rushwa, kusisitiza kujitegemea na uzalendo kwa nchi.
“Kazi za kawaida kweli zinafanywa na zinaendelea, lakini sina uhakika hata kidogo kama uadilifu aliotuachia Mwalimu bado tunao, sijui nani wa kulaumiwa,” alisema Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa. Alisema kwa namna ambavyo mambo yanakwenda, ni kiashiria tosha kuwa nchi haina uadilifu tena.
“Mambo yanavyokwenda kama gari lililo katika usukani,” alieleza Mwinyi na kuongeza kuwa kuna kila sababu ya kutafakari hali ilivyo sasa ikilinganishwa na ile ambayo iliachwa na Baba wa Taifa miaka hiyo 17 toka kufa kwake.
Alisema nafasi hiyo ya mazungumzo katika mdahalo, inawapasa kukaa kutafakari namna ya kurudisha nchi kwenye reli ambayo iliachwa na Mwalimu Nyerere ambaye ndiye muasisi wa taifa hili katika misingi ya uongozi.
“Tuna utajiri wa machoni, lakini ndiyo aliyokusudia Mwalimu? Alitufundisha tuwe matajiri wa vitu au matajiri wa moyo? Tujali vitu au tujali utu?” Alihoji Rais huyo mstaafu.

No comments:

Post a Comment