Showing posts with label Cuf. Show all posts
Showing posts with label Cuf. Show all posts

Wednesday, October 12, 2016

Maalim Seif kaandika barua kwenye Benki zote nchini kuzuia Profesa Lipumba kufungua akaunti kwa jina la Chama

Kukiwa bado kuna mkanganyiko wa kisiasa kwenye chama cha CUF sasa Katibu  Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, amemdhibiti mwenyekiti anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba kwa kuandika barua kwa benki zote ili kudhibiti ruzuku ya chama isipite kwenye mikono ya kiongozi huyo.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kumtambulisha Prof. Lipumba Benki ya NMB Tawi la Ilala akitaka apewe ushirikiano wa kufungua akaunti mpya ya chama.

Taarifa kutoka ndani ya CUF zinasema kuwa juzi Maalim Seif, aliandika barua kwa benki zote kuzuia hatua hiyo kwa kuweka zuio la mtu yeyote kufungua akaunti ya chama.

“Unajua hii vita si ya kitoto ni mapambano yaliyopo ndani ya CUF lakini yana nguvu kubwa kutoka katika kila pembe ya watu wanaochukia upinzani. Na pia wapo hata viongozi wakubwa wa dola ambao kila siku wamekuwa wakifanya kazi ya kuivuruga CUF.

“Walitegemea lakini tangu jana (juzi) Katibu Mkuu ameziandikia barua benki zote nchini kuzuia mpango wa Msajili kutaka kuchepusha ruzuku ya chama na kwenda katika mikono ya Lipumba na sasa nakala yake imepelekwa kwa Msajili wa Vyama,” alisema mtoa habari wetu.

Hatua ya Profesa Lipumba kufungua akaunti inatokana na barua aliyopewa na Msajili wa Vyama vya Siasa ya Oktoba 6, mwaka huu iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kwenda kwa Meneja wa Benki NMB Tawi la Ilala.

Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba HA.322/362/14/104  inamtambulisha Profesa Lipumba kutakiwa kufungua akaunti mpya ya The Civic United Front (CUF).

Siri ya Profesa Lipumba kutaka kufungua akaunti mpya yenye jina la Chama cha Wananchi CUF inadaiwa kutolewa na watumishi wa benki wa tawi hilo.

Prof. Lipumba ni Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, huku chama chake kikiwa tayari kimemfukuza uanachama.

Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kupitia Sisty Nyahoza ilinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikikiri kumtambulisha Profesa Lipumba kwa Benki ya NMB ili aweze kufungua akaunti hiyo, hata hivyo ikikana kujua matumizi ya akaunti hiyo.

Monday, October 10, 2016

CUF Wapata kibali kutoka Mahakama kuu Kufungua Kesi Dhidi ya Msajili wa Vyama na Lipumba

Wakati taariza zinazomtuhumu Profesa Ibrahim Lipumba kufungua akaunti benki kwa lengo la kuingiziwa fedha za ruzuku ya Chama cha Wananchi (CUF) kinyume cha sheria kwa ajili ya kukivuruga chama hicho zikienea.
Bodi ya Wadhamini ya CUF imetoa onyo pamoja na kuwatahadharisha watu wanaotumika kusaini nyaraka feki kwa lengo la kufungua akaunti hizo, pia imezitahadharisha benki zote nchini kutofungua akaunti yoyote kwa jina la CUF pasipo kupata muhtasari wa bodi halali ya chama hicho.
Katika hatua nyengine, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro amefafanua kuwa wenye mamkaka halali ya kufungua akaunti ya chama hicho ni Bodi yake ya wadhamini pamoja na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi.
“Tunatoa onyo, kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kwamba tumeshafungua shauri na utaratibu wa kisheria umeshaanza kuchukua mkondo wake, tumesikitika kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, kinyume cha sheria namba tano 1992 ya vyama vya siasa na kinyume cha katiba, Msajili kwa mara ya kwanza anaziandikia benki zilizosajiliwa na BOT akizitaka kumfungulia akaunti Lipumba za kuwekea fedha,” amesema Mtatiro.
Mtatiro amedai kuwa ”Benki itakayomfungulia akaunti Lipumba ni makosa makubwa. Sababu huwezi fungua akaunti ya taasisi au chama bila ya bodi yake ya wadhamini kukaa kikao na kuandaa muhtasari kwa ajili ya kupeleka benki ili kufungua akaunti.Lipumba na watu wake wameandaa nyaraka feki pamoja na barua ya msajili kutaka kufungua akaunti. Tunajua amepeleka katika benki mbalimbali,
“NMB ilikataa sasa wanapeleka benki ya Exim na ilishapewa taarifa kuwa uhuni huu haukubaliki na masuala ya fedha yako chini ya katibu mkuu kwa mujibu wa katiba ya cuf,” amesema.
Sambamba na onyo lililotolewa na bodi hiyo, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam leo imekubali maombi yake ya kufungua shauri la kuitaka mahakama hiyo kutoa amri dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi ya kutoendesha shughuli zake za usimamizi wa vyama vya siasa kinyume cha sheria, pamoja na kutengua barua yake inayomtambua profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha maombi hayo, Wakili Juma Nassoro amesema kuwa Jaji wa mahakama hiyo Munisi, amekubali maombi yao na kwamba jopo la mawakili wa CUF linatarajia kuwasilisha maombi rasmi wiki hii.
“Jaji Munisi baada ya kutusikiliza vifungu vya sheria tulivyotumia, Mahakama imekubali ombi letu ili tuweze kufungua maombi ya kuomba mahakama itamke kufuta barua ya msajili inayomtambua Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF. Pia Itoe zuio rasmi kwa msajili kutofanya shughuli zake nje ya utaratibu ambao amepewa chini ya sheria ya vyama vya siasa,” amesema Nassoro.
Amesema baada ya mahakama kuridhia maombi yao, iliwataka kuwasilisha maombi rasmi ndani ya siku14 kuanzia leo.
“Tumeambiwa tuwasilishe maombi ndani ya siku 14, lakini tutayawasilisha ndani ya siku Saba na tutaiomba mahakakama iyasikilize kwa Hati ya dharula ili shughuli za chama ziendelee,”amesema.

Sunday, October 9, 2016

Ninayo taarifa ya umoja wa Vijana wa CUF (JuviCUF) kutangaza Kususia Ziara ya Profesa Lipumba Mikoa ya Kusini

Ikiwa bado kuna mkanganyiko wa mambo ndani ya chama cha CUF, Umoja wa Vijana wa CUF (JuviCUF) umewataka vijana wa chama hicho kutotoa ushirikiano kwenye ziara ya mwenyekiti aliyevuliwa uongozi na Baraza Kuu, Profesa Ibrahim Lipumba na baadhi ya wabunge inayotarajiwa kuanza wiki hii mikoa ya Lindi, Mtwara na Tanga.

Wito huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Juvi-CUF, Hamidu Bobali alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa ziara hiyo ina lengo la kukipasua chama hiko rasmi.

“Tunajua ziara hiyo inataka kuongeza mpasuko ndani ya chama na mpasuko huo utawapa mwanya maadui zetu ‘kutupiku’ kisiasa,” alisema Bobali.

Bobali, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga kwa tiketi ya chama hicho, alisema pamoja na harakati za Lipumba tayari wabunge wa mikoa hiyo wapo katika kikao kuandaa mikakati ya kuimarisha chama.

Kadhalika Bobali alifafanua kuwa kama Jumuiya wanalaani kitendo kilichofanywa na kikundi cha vijana kilichojiita cha Mkoa wa Dar es Salaam cha kutoa kashfa kwa viongozi wa Ukawa akiwamo Freeman Mbowe na Julius Mtatiro.

Juvi-CUF iliwatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuhusu hali ya kisiasa iliyopo visiwani humo, kutokana na hatua mbalimbali za kisheria zinazofuatwa ili kuhakikisha haki inapatikana kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kuhusu sakata la akaunti ya chama inayoingizwa fedha za ruzuku na za wabunge, alisema hakuna fedha za wabunge zitakazoingia katika akaunti hiyo kutokana na mikataba inayosainiwa inahusu Mbunge na Ofisi ya Bunge na siyo chama.

“Tumechukua hatua kuwaeleza benki kuhusu akaunti kufunguliwa, suala hili linafanywa na bodi ya wadhamini inayoongozwa na Khatau hivyo siyo suala rahisi yeye (Lipumba) akazipata,” alisema Khatau.