Showing posts with label Habari za biashara. Show all posts
Showing posts with label Habari za biashara. Show all posts

Friday, October 14, 2016

Kuhusu ishu ya makontena 100 kupitishwa Bandarini bila kukaguliwa, Waziri mwaijage katoa muda mchache wa wahusika kujisalimisha


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ametoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena 100 bandarini bila kukaguliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wakatoe taarifa katika shirika.
Mwijage alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupata taarifa kuwepo kwa makontena 100, yaliyotolewa bandarini kwa siku zilizopita bila kukaguliwa na TBS.
“Nawataka wafanyabiashara wote waliochukua kontena hizo, wajisalimishe haraka TBS kabla ya kufika Jumanne ili wakaguliwe. Najua kuanzia kesho (leo) ni mapumziko, lakini TBS itaweka dawati la kuwasikiliza mpaka Jumatatu na ikifika Jumanne hatua zitachukuliwa kwa wahusika wote,” amesema Mwijage.
Alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15.
Aidha, alisema kwa mawakala wa forodha wote, waliohusika kutoa kontena hizo wizara yake itawasiliana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ili kuona hatua za kuchukua kwa kuwa serikali haiwezi kukubali mchezo huo.
“Tayari tulishafunga michezo ya namna hii na tumeanza maisha mapya kwa hiyo mawakala na wote mliohusika kutoa kontena hizo sababu hazijafika mbali tunaomba mtueleze zilipo ili tukazikague,” aliongeza.
Pia alisema kontena hizo zilipaswa kukaguliwa na TBS, lakini baada ya tukio hilo kontena hizo zitakaguliwa na shirika hilo wakishirikiana na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC).
 Aidha, amewaagiza TBS na FCC wafuatilie watu wao na kuziona bidhaa hizo, kwani watakaoshindwa hawatapewa cheti cha ubora bila kuona bidhaa na kukaguliwa.
“Sisi hatutaki mje mtueleze ni mzigo kiasi gani ili tupige penati hapana tunataka hilo kontena mlione na hiyo bidhaa muione na mkague,”aliongeza waziri huyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Egid Mubofu alisema ni vyema wafanyabiashara hao wakafuata maagizo hayo na kujitokeza kukaguliwa ilikuepuka faini hiyo ya asilimia 15. 
Alisema upitishaji wa bidhaa bila kukaguliwa na shirika hilo unaweza kuleta madhara makubwa kwa watumiaji ambao hawajui kama bidhaa yako imekaguliwa ubora.
“Najua wafanyabiashara wengine watasema hatuendi kukaguliwa sababu hataitumia bidhaa hiyo, lakini anasahau kama anaweza siku moja na yeye akatumia bidhaa hiyo ambayo haijakaguliwa ni vyema wakawa wazalendo na kufuata maagizo waliyopewa,” alisema Mubofu.
TBS imeanzisha utaratibu mpya wa kulipisha faini mizigo inayoingia hapa nchini, ambayo haikukaguliwa wakati iko nchini China. Faini ni asilimia 15 ya thamani ya mzigo ulioingia.

Tuesday, October 11, 2016

Kampuni ya Bakhresa Kujenga Viwanda Zaidi Vya Matunda, Vyakula.

Kampuni ya Bakhresa Foods imedhamiria kuongeza viwanda vingine vya usindikaji matunda hapa nchini ili kuongeza thamani kwa mazao ya wakulima.
Ahadi hiyo imetolewa leo (Jumanne, Oktoba 11, 2016) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Said S. Bakhersa wakati alipokutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kufanya naye mazungumzo ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Bw. Bakhresa amesema wana mpango wa kujenga kiwanda kimoja kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na kwamba wamefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watu wanapata usumbufu wa kusafirisha matunda hadi Dar es Salaam ndipo wayauze.
“Kuanzia tarehe 15 Oktoba, tutaanza kupokea matunda kutoka Kahama na maeneo ya jirani, na kwa siku tunapata semi trela zaidi ya 30. Yakimalizika ya kule tunaanza kupokea mengine kutoka mikoa ya Pwani na Kusini.”
“Tukijenga kiwanda Kanda ya Ziwa, tutapunguza adha ya wadau kusafirisha matunda kutoka kule hadi hapa kiwandani na badala yake sisi tutakuwa tunasafirisha concentrated juice na kuileta hapa kwa hatua zaidi za usindikaji,” amesema.
Amesema wana mpango wa kuendeleza usindikaji wa vyakula vya nafaka kwenye mikoa ya Kusini na kwamba hadi sasa wameajiri wafanyakazi zaidi ya 8,000 wakiwemo Watanzania 180 ambao wameajiriwa kwenye matawi yake nje ya nchi. “Hawa tunawalipa kamaexpatriates,” amesisitiza.
Amesema hivi sasa Kampuni hiyo imekwishafungua matawi mengine kwenye nchi za Rwanda, Burundi, Msumbiji, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Kampuni ya Bakhresa Foods inatengeneza vyakula mbalimbali zikiwemo juisi, soda, maji, biskuti, ice-cream, vyakula vya nafaka kama ngano, mahindi, mchele na bidhaa za kuokwa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu amemhakikishia Bw. Bakhresa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano kushirikiana na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kwani imedhamiria kukuza uchumi wa Tanzania kupitia uzalishaji wa viwandani.
“Serikali inathamini mchango wa wenye viwanda katika nchi yetu. Tunawashukuru ninyi ambao ni wakongwe kwenye sekta hii, na kwa hiyo tunawaomba msikate tamaa, muendelee kufungua viwanda zaidi ili wananchi wetu wapate mahali pa kuuzia mazao au bidhaa zao,”amesema.
Amemuomba Bw. Bakhresa aangalie maeneo mengine zaidi ya kuwekeza kama vile sekta za hoteli na utalii ili kusaidiana na Serikali kukuza uchumi wa Tanzania.
IMETOLEWA NA:OFISI YA WAZIRI MKUU,JUMANNE, OKTOBA 11, 2016.

Monday, October 10, 2016

Takwimu zimeonyesha kupungua kwa mfumuko wa bei Tanzania...

Ofisi ya taifa ya Takwimu imetoa Taarifa ya Mfumuko wa bei kupitia ofisi zake zilizopo Posta jijini Dar es salaam, ambapo ofisi hiyo ya taifa ndiyo pekee yenye mamlaka ya uchambuzi  , ukusanyaji pamoja na utoaji wa Takwimu rasmi kwa mujibu wa sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
Mfumuko wa bei wa taifa kwa kipimo cha mwaka ambao unapima kipimo cha mabadiliko ya  bei za bidhaa na huduma zote  zinazotumika na kaya binafsi. Mfumuko wa bei  za taifa  kwa mwezi Septemba, 2016 umepungua hadi asilimia 4.5  kutoka asilimia 4.9 iliyokuwa mwezi uliopita. Hii ina maanisha  kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa  fahirisi za bei zimeongezeka  hadi 103.05 mwezi Septemba 2016 hadi kufikia 98.64 kwa mwezi septemba 2015 , mfumuko wa bei ya vyakula  na vinywaji baridi umepungua hadi asilimia 6.0 kutoka asilimia 7.0 mwezi Agosti mwaka huu. Kupungua kwa mfumuko wa bei  ya mwezi Septemba  kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi septemba 2016 zikilinganishwa na bidhaa mwezi uliopita.
Lakini pia thamani ya shilingi ya Tanzania mwezi septemba 2016  kutokea mwezi disemba 2015 inaonesha uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia shilingi 97 na senti 04 mwezi Septemba 2016 kutokea mwezi Disemba mwaka jana ni shilingi 93 na senti 83 kwa ilivyokuwa mwezi Agosti 2016.
Kwa nchi jirani na baadhi ya nchi za Afrika huko nchini Kenya mfumuko wa bei za bidha mwezi uliopita umeongezeka kidogo hadi asilimia 6.34  kutoka asilimia 6.26 , kwa Uganda mfumuko wa bei  umepungua hadi asilimia 4.2 kutoka asilimia 4.8 mwezi Agosti.

Saturday, October 8, 2016

Bodi ya Mikopo (HESLB ) Yasitisha Mikopo Ya Walimu Wanafunzi Waliompiga Mwanafunzi Mbeya

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inautaarifu umma kuwa imesitisha mikopo ya elimu ya juu iliyokuwa ikitolewa kwa walimu-wanafunzi wanne waliosimamishwa masomo kwa kuhusika katika tukio la kumshambulia na kumuumiza mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya. Walimu hao walikuwa katika mafunzo ya vitendo.

1. Frank Msigwa - Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE)

2. John Deo- Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE)

3. Evance Sanga - Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE)

4. Sante Gwamaka - Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA)

Kwa utovu huo wa nidhamu, wanafunzi hao wamesimamishwa masomo na mamlaka husika kwa hiyo wamepoteza sifa za kuendelea kupokea mikopo. 

Mikataba inayosainiwa na wanufaika wa mikopo inawataka wanufaika kuzingatia masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na nidhamu na kufuata sheria na taratibu za vyuo na mamlaka halali.

Aidha, kwa mujibu wa taratibu za kukopeshwa, wanafunzi hawa watatakiwa kuanza kurejesha kiasi walichokopeshwa mara moja.

Bodi ya Mikopo inawakumbusha wanufaika wanaoendelea masomo kuzingatia masharti ya ukopeshwaji na kuheshimu sheria, kanuni taratibu na kuwa mfano mwema katika jamii. Mikopo na ruzuku zinazotolewa na Serikali ni kwa ajili ya kuwaandaa kuwa raia wema, waadilifu, na wachapa kazi ili kujenga uchumi imara na ustawi kwa wote.

Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru
Mkurugenzi Mtendaji

Ijumaa, Oktoba 7, 2016

Hapa ni tarehe rasmi ya Ndege za ATCL kuanza safari zake...


Ndege za ATCL zinataraji kuanza safari zake kuanzia tarehe 15 oktoba mwaka huu.
ATCL ambayo ina ndege tatu sasa hivi zitaanza safari za Mwanza, Arusha, Zanzibar, Kigoma, Tabora, Mbeya, Mtwara, Kilimanjaro, Bukoba, Dodoma na Mpanda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika hilo pia ndege hizo zitafanya safari kwenda Comoro, Nairobi na Entebbe.
Chanzo: Mwananchi.

Friday, July 29, 2016

Tayari ratiba ya treni mpya Dar imetoka jijini Dar es Salaam


Uongozi wa kampuni ya reli Tanzania ‘TRL’ umetangaza kubadilishwa kwa muda wa kuondoka treni ya abiria kutoka Dar es salaam kwenda bara kuanzia August 02 2016, ambapo treni itaondoka saa 9 alasiri badala ya saa 11 jioni ilivyozoeleka.
Mabadiliko hayo yamefanyika ili kutoa nafasi kwa treni ya pili ya huduma ya jiji kutoka kituo kikuu cha reli cha Dar es salaam kwenda Pugu ambayo itaanza kutoa huduma Jumatatu Agosti Mosi, 2016.
Aidha huduma mpya ya treni ya jiji kwenda Pugu itakuwa na vituo 10 kama ifuatavyo,Pugu stesheni, mwisho walami, Gongo la mboto, FFU Mombasa, Banana njia panda kwenda Segerea) na Karakata, vingine ni pamoja na Vingunguti Mbuzi, SS Bakhressa, kamata na kituo kikuu cha reli Dar es salaam.
Huduma ya treni imeelezwa itakuwa ya awamu mbili asubuhi na alasiri ambapo treni ya kwanza itaondoka kituo cha Pugu saa 12 asubuhi na kuwasili kituo cha Dar es salaamsaa 12:55 asubuhi na kufanya safari 3 zitakazomalizika saa 05:15 asubuhi.
Jioni pia kutakuwa na safari 3 ambapo treni ya kwanza itaondoka kituo cha Dar es salaamsaa 09:55 alasiri kwenda pugu na kuwasili saa 10:50 jioni na safari ya mwisho kutoka Pugu kwenda Dar es salaam itakuwa saa 03:20 usiku.