Friday, January 27, 2017

Geita: Watu 14 wafukiwa na kifusi mgodini


Watu kumi na nne wamefukiwa na udongo Alhamisi hii baada ya mgodi mmoja kuporomoka katika mkoa wa Geita, walipokuwa wakiendelea na uchimbaji wa madini.
Watu hao ni raia 13 Watanzania na raia mmoja wa China. Tukio hilo limetokea saa 9 usiku leo (jana) wakati wachimbaji hao wakiendelea na shughuli ya uchimbaji katika mgodi wa RZ unaomilikiwa na wachina.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga ametembelea eneo la tukio na kuona shughuli za uokozi zikiendelea na kuagiza nguvu ziongezwe.
Inaelezwa kuwa udongo umeporomoka kutokana na mgodi kuchimbwa zamani na Wajerumani hivyo kusababisha baadhi ya maeneo hayo kuwa na nyufa na vyuma kushindwa kushikilia udongo wa juu hali ambayo imesababisha kuzidiwa na hatimaye kuporomoka.
Kamisha msaidizi wa madini kanda ya ziwa victoria Mhandisi Yahaya Samamba amesema jitihada zilizofanyika ni kuwasiliana na migodi iliyopo karibu na eneo hilo pia wameomba msaada kutoka Kahama na kwenye mgodi wa GGM kupatiwa vifaa vya uokoaji ili zoezi hilo liweze kufanikiwa.
“Jitihada ambazo tumezifanya hadi sasa tumeomba msaada Kahama na kwenye mgodi wa Geita,kupatiwa vifaa ambavyo vitasaidia kwa wepesi zoezi hili la uokoaji ingawa tumeshapata vifaa vingine kutoka kwenye mgodi wa Busolwa”,alisema Samamba.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita Elisa Mugisha amesema eneo la chini ambalo limefukiwa na udongo ndiyo ambalo sasa wanaendelea kulitanua ili sehemu hiyo iwe kubwa watu waweze kupita.
“Eneo lote lile la chini limefukiwa na udongo lakini kule chini kunaonekana kuna sehemu za kwenda pembeni ingawa limefukiwa lakini chini kuna uimara kuna uwezekano kule chini wale watu wapo hai na wamepelekewa mipira ya hewa na kazi inayofanyika ni kutanua eneo ambalo litasaidia kuwatoa watu hao”,amesema.
Mwanasheria na msemaji wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya RZ Frances Kiganga ameelezea kuwa chanzo kikubwa ni mashimo ya zamani kwani udongo unapotikisika umekuwa ukisababisha baadhi ya nyufa kuendelea kupata shida.

No comments:

Post a Comment