Hapa nazungumza na wale ambao wanatamani kuwa waaminifu kwa wapenzi wao. Yapo mambo mengi, lakini hapa ninajitahidi kueleza yale ya muhimu zaidi. Wiki iliyopita niliishia kwenye kipengele cha mitandao ya kijamii, kwa kuwa sikukimaliza, tutaendelea hapo.MITANDAO YA KIJAMII
Utafiti usio rasmi unaonesha kwamba, pamoja na kwamba mitandao ya kijamii imesaidia kwa kiasi kikubwa sana kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kuendesha mijadala na kukuza ufahamu wa mambo mengi, suala la mapenzi limetajwa!
Utakutana na mtu Facebook (mfano), mmekuwa marafiki, lakini siku ya siku anaanzisha mambo ya mapenzi. Kwa sababu umeshakuwa naye karibu kwa muda mrefu, umekuwa wazi kwake ni rahisi kuanguka!
Hisia za mapenzi wakati mwingine hudanganya. Ngoja niwaambie ukweli, unapokuwa unawasiliana sana na mtu wa jinsi tofauti na yako, hisia za mapenzi huwa kali sana, kiasi kwamba ukiambiwa tu unapendwa, ni rahisi kuingia mkenge!
Kwenye mitandao ya kijamii kwa mfano Facebook, BBM, Twitter na mingineyo maarufu kuna utamaduni wa kuweka picha. Wakati mwingine picha hudanganya...kwa haraka haraka mtu eti anasema amekupenda. Hakuna lolote zaidi ya kuwaza ngono tu!
Huo ndiyo ukweli. Tatizo ni kwamba, huwezi kujua kama kuna hatari hiyo mbele yako. Unao marafiki wengi, mnataniana kila wakati, siku akilianzisha, inakuwa ngumu kuchomoka. Hata hivyo, kuna mambo madogo sana ukiyafanya yatasaidia kukutoa kwenye mtego.
Utakuta mtu ana mpenzi wake, mke au mume. Kifupi yupo kwenye uhusiano, lakini kwenye mtandao anaandika yupo ‘single’. Kwa nini hutaki kujulikana kuwa upo kwenye uhusiano?
Hujiamini? Humpendi mpenzi wako au tatizo ni nini hasa? Rafiki zako wanapoona huna mtu kwenye maelezo yako, wanatumia nafasi hiyo kukutega. Kwa nini ujiweke kwenye mitego? Kama upo kwenye uhusiano, kuwa mkweli, andika.
Ikiwezekana sehemu ya kuweka picha yako, weka ya mpenzi wako au mliyopiga pamoja, hii itasaidia marafiki kukuheshimu na wale wenye tabia za kipuuzi kujitoa mapema.
Wanaotumia mitandao ya kijamii ni mashahidi wa hiki ninachokizungumzia hapa.
MAVAZI
Kipengele hiki kinawagusa zaidi wanawake. Mavazi yanazungumza! Ulivyovaa ndivyo unavyojitafsirisha kwa wanaokutazama. Inawezekana ukawa ni mwaminifu kwa mwenzako na unajitahidi sana kuhakikisha unakuwa katika hali hiyo, lakini mavazi yako yanaweza kukutibulia.
Kwa nini uvae nguo zinazoonesha maungo yako ya ndani? Mchumba au mke wa mtu, kwa nini uvae vinguo vya ovyo? Unamwonesha nani sasa huko barabarani? Ndugu zangu, sijawahi kuona mwanamke aliyevaa kiheshima akapata usumbufu kwa wanaume njiani.
Hata kama unajijua huwezi kutegeka, lakini nataka kukuhakikishia kwamba, kusumbuliwa sana ni njia ya kuelekea kwenye usaliti. Ipo mifano hai; Kuna dada mmoja alikuwa anavaa vinguo vya kubana, kila akipita anasumbuliwa na mwanaume fulani hivi mtaani kwao.
Ameshamtumia watu mara nyingi, lakini anakataa. Siku moja ikatokea amehitilafiana na mpenzi wake, kwa hasira akaamini kuwa ameshaachana naye na hamtaki tena. Alipopita ile sehemu, yule jamaa akamuita.
Akilini mwake, akaona hakuna sababu ya kumtesa yule jamaa wakati amegombana na mpenzi wake. Kwa lengo la kujiliwaza akaenda, jamaa alilala naye siku hiyo hiyo! Alijuta baada ya kumaliza tendo!
Ya nini yote hayo? Vaa mavazi ya heshima. Jisogeze kwenye uaminifu. Ni nani atakayekusumbua ikiwa mavazi yako yanaonesha heshima uliyonayo?
Usikose wiki ijayo katika sehemu ya mwisho, kuna mambo mengi ya muhimu unayotakiwa kujua.